Pamoja na pesa ndefu wanayompa Sanchez, United bado namba 1 kwa utajiri duniani
Pamoja na kuanza kutoa kiasi cha £600,000 kila wiki kwa ajili ya nyota wao mpya Alexis Sanchez lakini hii haijawafanya Man United kuyumba kifedha na taarifa zinaonesha bado wako kilele cha klabu tajiri ulimwenguni.
Taarifa ya kifedha kutoka kwa shirika la Deloitte inaonesha kwamba Manchester United wanaongoza orodha ya vilabu tajiri ambapo kwa msimu 2016/2017 Manchester United wametengeneza kiasi cha £676.3m.
United wanakuwa wamewapiku Real Madrid kwa mara ya 10 na sasa Real Madrid wako nafasi ya pili kwani kwa msimu wa mwaka 2016/2017 matajiri hao wa Hispania waliweza kutengeneza pesa kiasi cha £674.6m.
Real Madrid wamekaa kwenye nafasi ya Barcelona na sasa Barca wameenda hadi nafasi ya tatu wakitengeneza kiasi cha £648.3m wakifuatiwa na mabingwa wa ligi ya Bundesliga waliotengeneza £587.8m.
Machester City vinara wa ligi kuu Uingereza wapo nafasi ya tano wakitengeneza mpunga wa £527.7m wakifuatiwa na Arsenal ambao 2016/2017 waliweka kibindoni jumla ya £487.6m.
Matajiri wa jiji la Paris(PSG) wako katika nafasi ya saba wakiwa wametengeneza pesa £486.2m, Chelsea wanafuatiwa na £428m, Liverpool £424.2m na Juventus nafasi ya 10 wanamalizia wakiwa wameingiza kiasi cha £405.7m.
Sanchez amponza Henry, mashabiki wataka sanamu lake livunjwe
Alexis Sanchez anazidi kuleta habari nyingi tangu ajiunge Manchester United, na sasa mshambuliaji huyo wa Chile amemuweka katika wakati mgumu mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Thiery Henry.
Moja kati ya mambo ambayo Sanchez amesema wakati akijiunga na Manchester United ni ushauri alioupata kwa Thiery Herny ambapo Sanchez amedai kuzungumza na Henry kabla ya kuondoka.
Sanchez amesema Thiery Henry aliona ni sawa tu kwa yeye kuondoka Arsenal na Sanchez aliamua kufuata ushauri wa Thiery Henry na kuamua kuondoka Arsenal.
Mashabiki mtandaoni hii leo wengi wamekuwa wakimtupia Henry lugha chafu na wengine wakisema hawataweza kumtambua tena Thiery Henry kama legend wa timu ya Arsenal.
Mashabiki wengi wamedai kwamba Henry amekuwa akiwageuka mara nyingi na wengine wakikumbushia kwamba juzi tu aliwahi kumsifia Harry Kane wakati Tottenham ni wapinzani wao.
Sasa mashabiki wa Arsenal toka pande mbalimbali duniani wamekuwa wakiomba klabu ya Arsenal kuvunja sanamu la mchezaji huyo lililoko nje ya uwanja wa Emirates kwa kuwa Henry ni msaliti.
Valverde kumtumia Coutinho kuiangamiza Espanyol
Tangu Phillipe Coutinho ajiunge na klabua ya Barcelona akitokea Liverpool hajaonekana uwanjani kuitumikia klabu yake hiyo mpya lakini siku ya Alhamisi huenda akakata kiu ya mashabiki wa Barcelona.
Barcelona watakuwa na mchezo wa Copa Del Rey siku ya Alhamis ambapo watambana na Espanyol huku kocha wa Barcelona Ernesto Valverde akithibitisha kwamba huenda Coutinho akawepo katika mchezo huo.
Usajili wa Coutinho uliigharimu Barcelona kiasi cha £142 m lakini kutokana na majeraha aliyotoka nayo Liverpool walishindwa kumtumia kiungo huyo wa Brazil.
Kuanzia katikati ya wiki iliyopita Phillipe Coutinho amekuwa akifanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha Barcelona na sasa kocha pamoja na madaktari wa timu hiyo wanaona yuko tayari kuanza kuitumikia Barcelona.
Katika mchezo uliopita Barcelona walifungwa bao moja kwa sifuri na Espanyol na kama wanahitaji nafasi ya kuendelea kuwepo katika michuano ya Copa Del Rey watahitaji kushinda mchezo wa Alhamisi.
Sahau kuhusu Sanchez, hawa wengine pia wamecheza chini ya Gurdiola na Mourinho
Leo kuna uwezekano mkubwa dili la Alexis Sanchez kwenda Manchester United kutoka Arsenal kukamilika, kama dili hii ikikamilika Sanchez atakuwa amecheza chini ya makocha wawili wakubwa EPL Pep Gurdiola na Jose Mourinho.
Kumbuka Alexis Sanchez kabla ya kwenda Arsenal, aliuzwa na Pep Gurdiola akitokea Barcelona lakini Sanchez hatakuwa mchezaji wa kwanza kucheza chini ya makocha hao wawili, wapo hawa nyota wengine.
Xabi Alonso, kwa misimu mitatu Xabi Alonso aliitumikia Real Madrid chini ya Mourinho lakini kipindi chote hicho Pep alitamani kumnunua Alonso na alipofika Bayern Munich mwaka 2014 alimvuta Xabi Alonso.
Zlatan Ibrahimovich, hii ni mara ya pili kwa Ibrahimovich kuwa chini ya Mourinho, mara ya kwanza ilikuwa Inter Milan lakini Zlatan pia alicheza chini ya Pep Gurdiola mwaka 2009 akiwa Barcelona na uhusiano wao inatajwa kuwa ulivurugika hapo.
Cesc Fabregas, wakati Fabregas akitoka Arsenal iliaminika kwamba anakwenda kuwa Xavi mpya ndani ya Barcelona lakini msimu wake mmoja tu ndani ya Barcelona ulibuma na baadaye Pep Gurdiola alimuuza kwenda Chelsea akakutana na Jose Mourinho.
Kevin De Bruyne, kati ya wachezaji ambao watu wa Chelsea wanamlaumu sana Jose Mourinho ni Kelvin De Bruyne, Mourinho hakuelewa uwezo wa Mbelgiji huyu na haikuwa kazi kwake kumuacha aende Ujerumani lakini baadaye Man City waliamua kumrudisha na sasa yuko chini ya Pep Gurdiola.
Pedro, hadithi ya Pedro na ya Fabregas zinafanana fanana kwani Pep Gurdiola ndiye alitoa ruhusa kwa Pedro kuondoka Barcelona ambapo aliitumikia tangu akiwa na timh B nyota huyo alikwenda Chelsea kukutana na Jose Mourinho.
Samuel Etoo, kama ilivyo kwa Zlatan Ibrahimovich, huyu naye alicheza chini ya Mourinho mara mbili akiwa na Inter na pia Chelsea lakini pia nyota huyu wa Cameroon amewahi kucheza chini ya Pep Gurdiola alipouzwa kwenda Barcelona.
Maxwell, alipokuwa Inter alikuwa chaguo la kwanza la Jose Mourinho katika beki ya kushoto lakini baada ya msimu mmoja tu Maxwell alivutiwa na kwenda Barcelona kwenda kucheza chini ya Pep Gurdiola.
Claudio Pizzaro, wakati Jose Mourinho akikaribia kuondoka Chelsea mwaka 2007 huu ulikuwa usajili wake wa mwisho mwisho lakini baada ya kucheza sana soka mwishowe Pizzaro aliamua kujiunga na Bayern Munich chini ya Pep Gurdiola.
Alexis(United), Mkhi (Arsenal) yametimia
Baada ya siku takribani 10 za mvutano, majadiliano na fununu hatimaye jioni ya leo suala la Alexis Sanchez na Henrikh Mkhitaryan kwenda Manchester United limekamilika.
United wamemtangaza rasmi Sanchez kama mchezaji wao ambapo raia huyo wa Chile atakuwa akiweka £600,000 kila mwisho wa wiki kutoka kwa wababe hao wa jiji la Manchester.
Wakati Sanchez akitangazwa kuwa mchezaji mpya wa United, nyota huyo amesema anafuraha sana kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Chile kuichezea klabu kubwa duniani.
Sanchez atakuwa anapokea mshahara wa £350,000 kila wiki huku akipewa kiasi cha £100,000 kila wiki itokanayo na haki za matangazo na pia atapewa bonus nyingine ya £140,000 kila wiki.
Wakati Sanchez akitangazwa na Manchester United hii leo, upande wa pili nako Henrikh Mkhitaryan ametangazwa na Arsenal kama mchezaji wao mpya.
Kwa mshahara wa Alexis sasa anakwenda kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika klabu ya Manchester United akiwa mbele ya Paul Pogba ambaye kwa sasa anapokea £220,000 kwa wiki.
Kwa upande wa Mikh aliyekwenda Arsenal amesema klabu hiyo ndiyo ilikuwa klabu ya ndoto zake na tangu akiwa mtoto mdogo alitamani siku moja kuvaa jezi ya Arsenal.