MRITHI WA DE GEA NJIANI KUTUA OLD TRAFFORD!!
Huku kukiwa na mipango ya chini chini ya Kipa Nambari Wani David de
Gea kurudi kwao Spain kuidakia Real Madrid, kumchukua Hugo Lloris
kunaelekea kuziba pengo hilo.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari hizi, Gazeti linaloheshimika huko
France L'Equipe, kilichobaki sasa ni mazungumzo ya kukubaliana Ada ya
Uhamisho na Mwenyekiti wa Tottenham Daniel Levy.
L'Equipe imedai Levy amemhakikishia Lloris kuwa Klabu yeyote
itakayotoa Ofa ya Pauni Milioni 18 kwenda juu basi atamruhusu kuhama
White Hart Lane.
Lloris, mwenye Miaka 28, alijiunga na Tottenham Mwaka 2012 akitokea Lyon ya France kwa Dau la Pauni Milioni 11.4.
Hata hivyo, Levy anasifika mno kwa ugumu wa kutoa Wachezaji wake Nyota na kama akiwaruhusu basi Dau lao huwa sio masihara.
UHAMISHO-OSPINA, NANI KUELEKEA UTURUKI? OBI NAE NJIANI UAE?
Ospina na Nani kutua Fenerbahce?
Kipa wa Arsenal, David Ospina, anedakia Timu ya Taifa ya Colombia,
ametoboa kuwa yuko kwenye mazungumzo na Klabu ya Uturuki Fenerbahce.
Kuondoka huku kwa Ospina ni kumpisha Kipa wa Chelsea Petr Cech
kuhamia Arsenal wakati kukiwa na ripoti kuwa Uhamisho huu uko njiani
kukamilika.
Ospina alihamia Arsenal Mwezi Januari akitokea Klabu ya France Nice
na kumvua Jezi Nambari Wani Wojciech Szczesny kwa kucheza Mechi 18 za
Ligi Kuu England.
Lakini ujio wa Cech na Szczesny kung'ang'ania kubaki Arsenal kumemfanya Ospina asake njia ya kwenda.
Wakati huo huo, Winga kutoka Ureno wa Manchester United, Nani,
mwenye Miaka 28, yupo njiani kujiunga na Fenerbahce ikiwa mazungumzo
kati ya Klabu hizo mbili yatakamilika.
Nani amepewa Ofa ya Mkataba wa Miaka Minne na Mshahara wa Pauni
55,000 baada ya Kodi na Fenerbahce ambayo iko tayari kuilipa Man UNited
Pauni Milioni 7 kwa Uhamisho wake.
John Obi Mikel
Baada kutupwa Benchi kufuatia uamuzi wa Meneja Jose Mourinho
kuwapendelea Viungo Nemanja Matic na Cesc Fabregas, Kiungo wa Nigeria
John Mikel Obi ameamua kutimkia UAE, Falme za Nchi za Kiarabu, na
kujiunga na Al Ain.
Obi alicheza chini ya nusu ya Mechi za Ligi wakati Chelsea wakitwaa
Ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita na hilo limemkera sana
Mnigeria huyo.