Simon Chimbo;
Mwezi Juni hadi Agosti ni miezi nyeti katika soka na hususan kwa wale
mashabiki wa ligi kubwa tano duniani. Miezi hii ni kipindi ambacho
timu, mashabiki pamoja na vyombo vya habari huwa macho kujua nani
anakwenda wapi na nani wanamhitaji.
Lakini swali hapa ni kwamba, kwanini ni ngumu kukuta katika picha za
nje za magazeti kipindi hiki cha usajili kuna sura za mabeki?
Mfano angalia ambavyo jina la Raheem Sterling, Harry Kane, Paul Pogba
na washambuliaji wengine yalivyotawala katika magazeti ya michezo?
Kwanini hatuoni mabeki? Ukiachilia mbali mlinzi wa Real Madrid, Sergio
Ramos na golikipa David de Gea wa Manchester United, bado hata bei zao
hazitajwi kuwa kubwa.
Sio kwamba walinzi hawasajiliwi, la hasha! Ila hawana thamani hii wanayopewa akina Paul Pogba na Raheem Sterling.
Kumbe mwisho wa haya yote tunapata jibu kwamba kumbe soka ni mchezo
wa matokeo. Ndio maana Liverpool wamemsajili mlinzi chipukizi wa
Southampton Nathael Clyne kwa pauni 12m huku wakimsajili mshambuliaji wa
brazil Roberto Firmino kwa pauni 29m.
Leo hii klabu ya Manchester United hawako tayari kutoa zaidi ya pauni
35m kwa mlinzi wa kati wa Real Madrid, Sergio Ramos lakini usishangazwe
wakitoa pauni 75m kwa mshambuliaji Gareth Bale wa klabu hiyo hiyo ya
Madrid.
Mpira ni mchezo wa ushindi, yaani magoli. Ndio maana sijashtushwa na
usajili wa pauni 12m wa mlinzi mbrazil kutoka Atletico Madrid, Miranda
wa kwenda Inter lakini nitashangaa kuona mshambuliaji wao Arda Turan
akiuzwa kwa pungufu ya pauni 25m.
Kimsingi hapa ni namna mfumo wa mpira unavyobadilika, katika ‘modern
game’ walinzi wamebadilishiwa majukumu na kwamba siku hizi mashambulizi
ya timu huanzia kwa mabeki. Walinzi wa pembeni siku hizi wamekuwa na
kazi ndogo zaidi ya ulinzi kuliko kushambulia kutokea pembeni.
Mlinzi Dany Alvez ameonekana mara nyingi katika nusu ya pili ya eneo
pinzani awapo uwanjani, lakini hali hiyo utaikuta pia kwa Philip Lahm wa
Ujerumani. Mpira ni magoli, ni ushindi. Ndio maana Barcelona walitoa
pauni 75m kumsajili Luis Suarez lakini kamwe hawawezi kutoa hata pauni
50m kumsajili mlinzi Diego Godin ama Vicent Kompany.
Hizo pamoja na sababu nyingine za matangazo ya kibiashara hufanya
timu kutoa macho zaidi kuwanunua wachezaji wa kiungo na ushambuliaji kwa
ada kubwa zaidi ya mabeki.
Thamani ya watu wa ulinzi inashuka na pengine ndio maana Sepp Blatter
alimpa tuzo ya mchezaji bora wa dunia Cannavaro wa Italia mwaka 2006
ili kujaribu kuinua thamani yao katika mchezo wa soka.
Pengine watu watasema hii ni Ulaya tu? Hapana ni kila sehemu ya dunia
hivi sasa. Kwani hatuoni magazeti yetu ya hapa bongo? Vichwa vya nje
vimepambwa majina ya akina Kaseke, Okwi, Busungu na Niyonzima, lakini
kwanini sio Oscar Joshua? Mpira ni magori, ushindi.