MASCHERANO: "WAMEMPIGA MATEKE NEYMAR NA KUMTUPA NJE!"
- Created: Saturday, 20 June 2015 16:19
Mascherano, ambae anacheza Klabu moja Barcelona na Neymar wa
Brazil, amedai Staa huyo hakulindwa na ametupwa nje ya Copa America.
Neymar alipewa Kadi Nyekundu na Refa wa Chile Enrique Osses baada
ya Mechi ya Kundi C la Copa America ambayo Brazil ilifungwa 1-0 na
Colombia Jumatano iliyopita kumalizika na Jana CONMEBOL, Shirikisho la
Soka la Nchi za Marekani ya Kusini, lilimfungia Mechi 4 ikimaanisha
hatacheza tena Mechi zilizobaki za Copa America.
Mascherano amesema kuwa kwa mara nyingine tena Waamuzi wamemwangusha Neymar.
Ameeleza: "Vitu kama hivi vinatokea tu kwenye Soka la Marekani ya
Kusini na hasa zaidi kwenye Copa America ambalo ni gumu kwa Wachezaji
kama Neymar wasiolindwa kama huko Ulaya. Neymar alipigwa Mateke mara 20
na badala yake akaonyeshwa Kadi ya Njano kwa kushika Mpira. Wachezaji
kama hawa wenye vipaji hawaruhusiwi kucheza. Wanashambuliwa sana na
kuumizwa. Lazima tufanye jitihada kuwalinda. Alipigwa Mateke mara 20.
Hili linakuathiri kichwani. Usisahau Neymar ni Neymar, ni Kijana wa
Miaka 23. Sasa Brazil wamepoteza sana!"
HABARI ZA AWALI
NEYMAR ATUPWA NJE COPA AMERICA!
Shirikisho la Soka la Nchi za Marekani ya Kusini, CONMEBOL,
limemfungia Kepteni wa Brazil Neymar Mechi 4 na hivyo kumtupa nje ya
Copa America ambayo Brazil inashiriki.
Kifungo hiki kinamaanisha Neymar ataikosa Mechi ya mwisho ya Brazil
ya Kundi C la Copa America na pia Robo Fainali na Nusu Fainali ikiwa
Brazil itafuzu.
Juzi, CONMEBOL awali ilimfungia Neymar Mechi 1 baada ya kupewa Kadi
Nyekundu Jumatano wakati Brazil inachapwa 1-0 na Colombia katika Mechi
ya Kundi C la Copa America huko Nchini Chile.
Kifungo hicho kilimfanya Neymar kuikosa Mechi ya mwisho ya Kundi C
watayocheza Jumapili dhidi ya Venezuela Mechi ambayo ni muhimu mno kwao
kufuzu kutinga Robo Fainali kwani Timu zote za Kundi hilo zimefungana
zikiwa na Pointi 4 kila mmoja.
Hata hivyo, wakati huo, Neymar alikuwa tayari aikose Mechi hiyo na
Venezuela kwani alikuwa ameshazoa Jumla ya Kadi za Njano mbili katika
Mashindano hayo.
Katika Mechi hiyo na Colombo, Neymar alionyeshwa Kadi Nyekundu na
Refa wa Chile Enrique Osses Mpira ukiwa umekwisha baada kumbabatiza na
Mpira Mchezaji wa Colombia Pablo Armero kitu ambacho kilizua rabsha na
Neymar kuonekana akijaribu kumpiga Kichwa Mchezaji mwingine wa Colombia.
Katika rabsha hizo, Mchezaji wa Colombia, Carlos Bacca, nae alipewa Kadi Nyekundu.
CONMEBOL ikitangaza Kifungo hiki cha Neymar imetamka kuwa wote, Neymar na Bacca, wana haki ya kukata Rufaa.
Mwaka 2014, huko Nchini kwao Brazil, Neymar alilazimika kuondoka
kwenye Fainali za Kombe la Dunia na kukosa Mechi zilizobakia baada ya
kupigwa Goti Mgongoni na Mchezaji wa Colombia Juan Zuniga na kuvunjwa
Mfupa wa Mgongoni bila ya huyo Zuniga kuadhibiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni