BAADA YA KUKATALIWA KUUZWA, BERAHINO AKATAA KUICHEZEA TENA WBA
Klabu ya Tottenham Hotspur ya
London ilikataliwa ofa zake tatu za kutaka kumsajili mshambuliaji huyo
mwenye miaka 22 ili amsaidie Harry Kane katika safu ya ushambuliaji ya
klabu hiyo.
Spurs walipeleka mara ya mwisho
dau la pauni 25m kwa kijana huyo mzaliwa wa Burundi aliyehamia Uingereza
na wazazi wake kutokana na vita ya Burundi, lakini mwenyekiti wa West
Bromwich bwana Jeremy Peace alikataa kata kata kumuachia mchezaji huyo.
Kuelekea kufungwa kwa dirisha la
usajili usiku wa tarehe 1 September, Saido Berahino kupitia ukurasa wake
wa Twitter aliandika kwa hasira kwamba anashindwa kutafuta maneno ya
kuelezea hisia zake, lakini akasema kamwe hatoichezea tena timu ya
Jeremy Peace akimaanisha West Bromwich.
Kwa takribani wiki tatu hivi
sasa, Saido Berahino hakua katika hali nzuri kiakili kutokana na kutaka
kuichezea klabu ya Tottenham Hotspur iliyokuwa ikimhitaji kwa udi na
uvumba, kitu kilichopelekea kocha wake Tony Pulis asimchezeshe katika
mechi zote tatu ilizocheza timu yake.
Tayari Tony Pulis ameeleza
kusikitishwa kwake na hali tete iliyopo kati ya Berahino na mwenyekiti
wake huku akisisitiza itakua kazi ngumu zaidi kurudisha mahusiano ya
Berahino na klabu kwa haraka.
Pulis amejitetea kwamba Tottenham
Hotspur walichelewa kuleta ofa nzuri na kwamba wao kama West Bromwich
wangeshindwa kupata mfungaji mwingine wa magoli na ndicho kilichopelekea
wao kutokuwa tayari kumuachia kijana huyo anaezungumza kiswahili
vizuri.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni