Mataifa matano yavutana kuandaa kombe la dunia 2030
Mashindano ya kombe la dunia ni jambo kubwa na muhimu sio tu kwa ajili ya soka bali kwa maendeleo ya nchi, tayari baadhi ya nchi zimeshaanza kupigana vikumbo kwa ajili ya kombe la dunia la miaka 13 ijayo.
Mataifa matatu kutoka America Kusini ya Argentina, Uruguay na Paraguay yamejiandaa kuungana na kuwa kitu kimoja kwa ajili ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo mikubwa duniani mwaka 2030.
Marais watatu Horacio Cartes kutoka Paraguay, Maurcio Macri wa Argentina na raisi wa Uruguay Tabare Vazquez waliweka kikao kwa pamoja na kujadili mambo mbali mbali ya mataifa hayo na ndipo wakaja na hoja moja ya kuungana.
Horacio Cartes amesema wiki ya kwanza ya mwezi November watatuma rasmi ombi lao na anaamini watapewa nafasi hiyo kwani itakuwa maalum kwa Uruguay kuadhimisha miaka 100 tangu mara ya mwisho kombe hilo kupigwa nchini humo.
Mwaka 1930 wenyeji wa michuano hiyo Uruguay wakiwa na kocha mwenyeji Horacio Supicci katika dimba la Estadio Centanario waliipiga Argentina mabao 4 kwa 2 na kubeba kombe hilo.
Hapo mwanzo Argentina na Uruguay ndio ambao walikuwa kitu kimoja kuandaa mashindano hayo lakini kikao kilichofanyika Beunos Aries kiliamua kuiongeza nchi ya Paraguay katika mpango huo.
Raisi wa chama cha soka duniani FIFA bwana Gianni Infantino ameipongeza Argentina kwa maamuzi yake hayo huku akiimwagia sifa kwamba ni moja kati ya mataifa ambayo yametengeneza historia kubwa katika soka.
Wakati Argentina, Uruguay na Paraguay wakijipanga kuaandaa mashindano hayo, huko barani Asia nchi ya China nayo imeonesha matamanio ya kuandaa michuano hiyo mikubwa duniani.
Ukiacha China lakini pia UEFA mwezi July mwaka huu walisema michuano ya mwaka 2030 ya kombe la dunia itakuwa jambo kubwa sana kwao na kusema kuwa wao kama Ulaya watawapa ushirikiano mkubwa Uingereza.
Michuano ijayo ya kombe la dunia itapigwa nchini Urusi mwakani huku baada ya hapo taifa la Qatar litaandaa michuano ya kombe la dunia mwaka 2022 na kisha Mexico – USA na Canada wakijipanga kwa 2026 ambapo Morocco nao wanaitaka.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni